Wako watu wengi ambao wametamani kuanzisha biashara zao wenyewe
au tayari wameshaanza biashara lakini hawana mpango juu ya biashara zao.Wazo la
kuwa bosi wewe mwenyewe na kujaribu kufanya biashara yako mwenyewe ili kujipatia
fedha zako mwenyewe linavutia sana.
Yawezekana wako watu ambao wana msukumo na uwezo wa kifedha wa
kuanzisha biashara lakini kikwazo kinachowakabili ni kujua aina ya biashara ambayo
itawapa faida.Wajasiriamali wengi hutumia muda mwingi kuchunguza,kuchanganua hivyo
kutokuwa na hakika ya wazo lipi kati ya hayo litawaridhisha zaidi na kuwa na ufanisi
zaidi.
Ili uwe na uhakika wa biashara unayofanya au unayotaka kuanzisha
ni muhimu uandike mpango wa biashara.Mpango wa biashara ni dira itakayokuelekeza
jinsi ya kuendesha na kusimamia vema biashara yako ili kupata mafanikio.
Mpango wa biashara ni
lazima uwe unatekelezeka na kueleweka vema
na mjasiriamali aliyeuandaa kwani yeye ndiyo mtekelezaji mkuu.
Mpango wa biashara ulioandaliwa kitaalamu na mshauri elekezi
ambao hautaeleweka na mjasiriamali hautaweza kutekelezeka na hivyo hauwezi kuleta
mafanikio katika biashara iliyokusudiwa.
Mpango wa biashara ni mpango unaoeleza mambo yote ambayo yatamsaidia
mjasiriamali husika kulifanyia kazi wazo lake la biashara kwa ufanisi zaidi.
Mpango wa biashara ni kama ramani ya barabara inayokuelekeza
wapi uelekee ili biashara yako iwe endelevu na kukua.Hujumuisha maelezo ya kimaandishi
juu ya biashara yako na takwimu za kifedha
zinazoonyesha gharama ya uendeshaji wa biashara yako.
Mpango wa biashara utamsaidia mjasiriamali kutambua nguvu na
udhaifu wa biashara yake na kutoa mkakati wa kuendeleza na kukuza biashara husika.
Mpango wa biashara pia husaidia biashara kukopeshwa fedha na
taasisi za kifedha kama mabenki ili kuongeza mtaji wa biashara.
Mpango wa biashara umegawanyika katika sehemu kuu nne.
Sehemu ya kwanza inahusu maelezo juu ya biashara husika.Maelezo
hayo ni jina la shirika au biashara husika,jina au majina ya wamiliki na aina ya umiliki ili kuonyesha kama
biashara inamilikiwa na mtu mmoja au kwa ubia.Aina ya biashara pia taarifa muhimu
katika kipengele hiki,ni muhimu useme ni aina gani ya biashara mfano biashara ya
kufungasha na kusambaza viungo,biashara ya kuuza nguo za watoto biashara ya kufuga
kuku wa mayai na kuuza mayai n.k.Eleza malengo ya biashara yako,bidhaa yako kwa
ufupi uonyeshe nani ni mnunuzi,mlaji wa mwisho kwa mfano usambazaji kwa mahoteli,mama
lishe,wanafunzi n.k.Elezea ubora wa bidhaa yako.Sehemu hii pia inajumuisha taarifa
za ofisi ilipo,gharama za pango,aina na idadi ya wafanyakazi na kazi wanazofanya,vyanzo
vya kupata wafanyakazi,na aina ya ajira kama wafanyakazi wa kudumu na wasio wa kudumu.
katika sehemu hii pia onyesha gharama ya vifaa au nyenzo za kazi,malighafi,gharama
zisizo za moja kwa moja kama kodi ya pango,gharama za umeme na maji,usafirishaji,mawasiliano
na gharama nyingine zote zisizo za moja kwa moja.
Maswala ya kisheria kama aina ya leseni,umiliki,usajili,mikataba
inaonyeshwa katika sehemu ya kwanza ya mpango wa biashara.
Sehemu ya pili ya mpango
wa biashara inahusu uchanganuzi wa soko.Soko ni wateja wa biashara yako na jinsi
au mahali wanapopatikana.Katilka sehemu hii jibu maswali yafuatayo.Kwa nini soko
linahitaji bidhaa yako?Soko litahitaji bidhaa kwa muda gani?kwani masoko yote hutokea
kutokana na mahitaji.masoko mengine ni ya msimu hivyo ni muhimu kufahamu,kwa mfano
kununua na kuuza mazao ni soko linaloendeshwa na misimu.Orodhesha tabia za wateja
wako na jinsi utakavyowahudumia,zingatia
umri/rika lao,mahali walipo,mtindo wa maisha(familia au wanafunzi),uwezo kiuchumi(wameajiriwa,wafanyabiashara,watu
wa kipato cha kati/cha chini au cha juu?Ni mambo gani wateja wako wanapendelea na
yapi hawapendelei?
Katika sehemu hii ni muhimu kuonyesha nguvu na udhaifu wa washindani
wako na jinsi utakavyoingia kwenye ushindani pamoja nao.Wachambue washindani kwa
majina na idadi yao,wajue washindani wa moja kwa moja na wale wasio wa moja kwa
moja.Tafuta kujua mapungufu ya washindani wako ili uutumie kama daraja la kuingia
sokoni.Chunguza kwa makini mahitaji ya soko ambayo washindani wako wameshindwa kutoa
huduma.
Katika sehemu hii jadili vichocheo vya kiuchumi,kisheria, kijamii
na kiteknologia vinavyoathiri soko lako. Kwa mfano kama wewe ni kinyozi tafuta kujua
jinsi ya kuboresha eneo la vifaa vya kazi kutokana na teknologia.Kama ni mjasiriamali
wa sekta ya usafirishaji boresha muonekano wa chombo chako cha usafiri.
Katika sehemu hii pia zingatia sana kuonyesha mkakati wako wa
kutafuta masoko na jinsi utakavyouza.Je utauza wewe mwenyewe au utatumia mawakala?Utatumia
mtandao au utatumia rasilimali watu kama baadhi ya makampuni yanavyofanya kuwapa
watu nidhaa zao wawauzie sokoni?
Sehemu ya tatu inaonyesha mpango wa usimamizi wa fedha.,ikijumuisha
taarifa ya fedha zitakazoingia na kutoka kwenye biashara yako.Katika sehemu hii
utaonyesha vyanzo vya fedha na matumizi ya fedha.Katika sehemu hii jumuisha taarifa
za uendeshaji ukionyesha mauzo,matumizi/gharama na faida au hasara.Anza kwa kuonyesha
mapato yote yanayotokana na uuzaji,mikopo,ufadhili,kuuza mali n.k.kisha jumlisha mapato yote.Onyesha matumizi
yote ya biashara kwenye malighafi,vifaa,mawasiliano,pango,mishahara,nishati,maji,marupurupu
ya wafanyakazi kisha jumlisha.Chukua jumla ya mapato utoe jumla ya matumizi.Kama
tofauti yake itakuwa chanya basi biashara imetengeneza faida,kama jibu ni hasi basi
biashara haikytengeneza faida.Tafuta kujua chanzo cha hasara ili ufanye marekebisho.Andaa
taarifa ya mapato na matumizi ya kila mwezi kwa mwaka mzima ili uone mwelekeo wa
biashara yako.Kwa kuanza unaweza kuandaa kwa miezi mitatumitatu.
Sehemu ya nne ni muhtasari ambao hueleza kwa ufupi taarifa muhimu
zinazopatikana katika mpango wa biashara.Japo sehemu hii huandaliwa mwishoni baada
ya kukamilisha mpango wa biashara ,huwa inatangulia
ukurasa wa mbele kama taarifa fupi juu ya mpango.Sehemu ya muhtasari itaonyesha
jina la biashara,wazo la biashara,historia na uzoefu wa biashara,taarifa za usajili,taarifa
za wamiliki na uzoefu wao,soko lililolengwa,faida ya biashara na jinsi itakavyokabiliana
na ushindani sokoni,matarajio ya biadhara na mipango ya siku zijazo ya kuendeleza biashara
yako.
Ni muhimu kwa kila mjasiriamali kuandaa mpango wa biashara ili
umuongoze katika utekelezaji wa wazo lake la biashara.Biashara bila mpango ni sawa
na kukosa dira.
No comments:
Post a Comment