Wednesday, October 28, 2015

MPANGO WA BIASHARA




 

Wako watu wengi ambao wametamani kuanzisha biashara zao wenyewe au tayari wameshaanza biashara lakini hawana mpango juu ya biashara zao.Wazo la kuwa bosi wewe mwenyewe na kujaribu kufanya biashara yako mwenyewe ili kujipatia fedha zako mwenyewe linavutia sana.
Yawezekana wako watu ambao wana msukumo na uwezo wa kifedha wa kuanzisha biashara lakini kikwazo kinachowakabili ni kujua aina ya biashara ambayo itawapa faida.Wajasiriamali wengi hutumia muda mwingi kuchunguza,kuchanganua hivyo kutokuwa na hakika ya wazo lipi kati ya hayo litawaridhisha zaidi na kuwa na ufanisi zaidi.
Ili uwe na uhakika wa biashara unayofanya au unayotaka kuanzisha ni muhimu uandike mpango wa biashara.Mpango wa biashara ni dira itakayokuelekeza jinsi ya kuendesha na kusimamia vema biashara yako ili kupata mafanikio.
Mpango wa biashara  ni lazima uwe unatekelezeka  na kueleweka vema na mjasiriamali aliyeuandaa kwani yeye ndiyo mtekelezaji mkuu.
Mpango wa biashara ulioandaliwa kitaalamu na mshauri elekezi ambao hautaeleweka na mjasiriamali hautaweza kutekelezeka na hivyo hauwezi kuleta mafanikio katika biashara iliyokusudiwa.
Mpango wa biashara ni mpango unaoeleza mambo yote ambayo yatamsaidia mjasiriamali husika kulifanyia kazi wazo lake la biashara kwa ufanisi zaidi.
Mpango wa biashara ni kama ramani ya barabara inayokuelekeza wapi uelekee ili biashara yako iwe endelevu na kukua.Hujumuisha maelezo ya kimaandishi  juu ya biashara yako na takwimu za kifedha zinazoonyesha gharama ya uendeshaji wa biashara yako.
Mpango wa biashara utamsaidia mjasiriamali kutambua nguvu na udhaifu wa biashara yake na kutoa mkakati wa kuendeleza na kukuza biashara husika.
Mpango wa biashara pia husaidia biashara kukopeshwa fedha na taasisi za kifedha kama mabenki ili kuongeza mtaji wa biashara.
Mpango wa biashara umegawanyika katika sehemu kuu nne.
Sehemu ya kwanza inahusu maelezo juu ya biashara husika.Maelezo hayo ni jina la shirika au biashara husika,jina au majina  ya wamiliki na aina ya umiliki ili kuonyesha kama biashara inamilikiwa na mtu mmoja au kwa ubia.Aina ya biashara pia taarifa muhimu katika kipengele hiki,ni muhimu useme ni aina gani ya biashara mfano biashara ya kufungasha na kusambaza viungo,biashara ya kuuza nguo za watoto biashara ya kufuga kuku wa mayai na kuuza mayai n.k.Eleza malengo ya biashara yako,bidhaa yako kwa ufupi uonyeshe nani ni mnunuzi,mlaji wa mwisho kwa mfano usambazaji kwa mahoteli,mama lishe,wanafunzi n.k.Elezea ubora wa bidhaa yako.Sehemu hii pia inajumuisha taarifa za ofisi ilipo,gharama za pango,aina na idadi ya wafanyakazi na kazi wanazofanya,vyanzo vya kupata wafanyakazi,na aina ya ajira kama wafanyakazi wa kudumu na wasio wa kudumu.
katika sehemu hii pia onyesha gharama ya vifaa au nyenzo za kazi,malighafi,gharama zisizo za moja kwa moja kama kodi ya pango,gharama za umeme na maji,usafirishaji,mawasiliano na gharama nyingine zote zisizo za moja kwa moja.
Maswala ya kisheria kama aina ya leseni,umiliki,usajili,mikataba inaonyeshwa katika sehemu ya kwanza ya mpango wa biashara.



Sehemu ya pili  ya mpango wa biashara inahusu uchanganuzi wa soko.Soko ni wateja wa biashara yako na jinsi au mahali wanapopatikana.Katilka sehemu hii jibu maswali yafuatayo.Kwa nini soko linahitaji bidhaa yako?Soko litahitaji bidhaa kwa muda gani?kwani masoko yote hutokea kutokana na mahitaji.masoko mengine ni ya msimu hivyo ni muhimu kufahamu,kwa mfano kununua na kuuza mazao ni soko linaloendeshwa na misimu.Orodhesha tabia za wateja wako na jinsi  utakavyowahudumia,zingatia umri/rika lao,mahali walipo,mtindo wa maisha(familia au wanafunzi),uwezo kiuchumi(wameajiriwa,wafanyabiashara,watu wa kipato cha kati/cha chini au cha juu?Ni mambo gani wateja wako wanapendelea na yapi hawapendelei?
Katika sehemu hii ni muhimu kuonyesha nguvu na udhaifu wa washindani wako na jinsi utakavyoingia kwenye ushindani pamoja nao.Wachambue washindani kwa majina na idadi yao,wajue washindani wa moja kwa moja na wale wasio wa moja kwa moja.Tafuta kujua mapungufu ya washindani wako ili uutumie kama daraja la kuingia sokoni.Chunguza kwa makini mahitaji ya soko ambayo washindani wako wameshindwa kutoa huduma.
Katika sehemu hii jadili vichocheo vya kiuchumi,kisheria, kijamii na kiteknologia vinavyoathiri soko lako. Kwa mfano kama wewe ni kinyozi tafuta kujua jinsi ya kuboresha eneo la vifaa vya kazi kutokana na teknologia.Kama ni mjasiriamali wa sekta ya usafirishaji boresha muonekano wa chombo chako cha usafiri.
Katika sehemu hii pia zingatia sana kuonyesha mkakati wako wa kutafuta masoko na jinsi utakavyouza.Je utauza wewe mwenyewe au utatumia mawakala?Utatumia mtandao au utatumia rasilimali watu kama baadhi ya makampuni yanavyofanya kuwapa watu nidhaa zao wawauzie sokoni?

Sehemu ya tatu inaonyesha mpango wa usimamizi wa fedha.,ikijumuisha taarifa ya fedha zitakazoingia na kutoka kwenye biashara yako.Katika sehemu hii utaonyesha vyanzo vya fedha na matumizi ya fedha.Katika sehemu hii jumuisha taarifa za uendeshaji ukionyesha mauzo,matumizi/gharama na faida au hasara.Anza kwa kuonyesha mapato yote yanayotokana na uuzaji,mikopo,ufadhili,kuuza mali  n.k.kisha jumlisha mapato yote.Onyesha matumizi yote ya biashara kwenye malighafi,vifaa,mawasiliano,pango,mishahara,nishati,maji,marupurupu ya wafanyakazi kisha jumlisha.Chukua jumla ya mapato utoe jumla ya matumizi.Kama tofauti yake itakuwa chanya basi biashara imetengeneza faida,kama jibu ni hasi basi biashara haikytengeneza faida.Tafuta kujua chanzo cha hasara ili ufanye marekebisho.Andaa taarifa ya mapato na matumizi ya kila mwezi kwa mwaka mzima ili uone mwelekeo wa biashara yako.Kwa kuanza unaweza kuandaa kwa miezi mitatumitatu.
Sehemu ya nne ni muhtasari ambao hueleza kwa ufupi taarifa muhimu zinazopatikana katika mpango wa biashara.Japo sehemu hii huandaliwa mwishoni baada ya kukamilisha mpango  wa biashara ,huwa inatangulia ukurasa wa mbele kama taarifa fupi juu ya mpango.Sehemu ya muhtasari itaonyesha jina la biashara,wazo la biashara,historia na uzoefu wa biashara,taarifa za usajili,taarifa za wamiliki na uzoefu wao,soko lililolengwa,faida ya biashara na jinsi itakavyokabiliana na ushindani sokoni,matarajio ya biadhara  na mipango ya siku zijazo ya kuendeleza biashara yako.
Ni muhimu kwa kila mjasiriamali kuandaa mpango wa biashara ili umuongoze katika utekelezaji wa wazo lake la biashara.Biashara bila mpango ni sawa na kukosa dira.

Thursday, October 15, 2015